Hali ya afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Dk. Steven Ulimboka inaendelea kuimarika licha ya maumivu makali yanayomkabili.
Akizungumza kwa taabu kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwenye Kitengo cha Mifupa (MOI) Dk. Ulimboka alisema, “Namshukuru Mungu naendelea vizuri tofauti na nilivyofikishwa hapa bado nina maumivu makali naomba kama kuna watu wanataka kuja kuniona wasije ili nipumzike,” alisema.
Awali Ofisa Uhusiano wa MOI Jumaa Almas alisema hali ya Dk. Ulimboka inaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa kwa kuwa sasa ana uwezo wa kutambua watu wanaofika kumjulia hali na kuzungumza kidogo.
“Kwa sasa hali yake ni nzuri na yuko chini ya uangalizi wa jopo la madaktari linaloongozwa na Professa Joseph Kahamba,” alisema.
Kuhusu mgomo katika kitengo hicho Almas alisema ni huduma za dharura pekee zinazotolewa huku zile za kawaida zikiwa hazifanyiki kabisa.
Dk. Ulimboka alifikishwa hospitalini hapo baada ya kutekwa na watu wasiojulikana kisha kumpiga,na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kutupwa kwenye msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo wa madaktari unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono akiwa amejeruhiwa vibaya.
No comments:
Post a Comment