RAIS Jakaya Kikwete ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za kuunganisha umeme.Amelitaka kufanya hivyo ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa kupata huduma hiyo akisema ikibidi, lifidie gharama hizo katika bili linazotoza kwa mwezi.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi kwa Taifa. Hotuba hiyo ilijikita katika mambo makuu matatu; ziara zake katika wizara, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mchakato wa Katiba mpya.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, gharama za kuunganisha umeme zinazotozwa na shirika hilo sasa, zinawafanya wananchi wengi washindwe kupata huduma hiyo."Nimewakumbusha pia kuwa tunalo lengo la kuwapatia umeme asilimia 30 ya Watanzania ifikapo 2015.
Lengo hilo halitafanikiwa iwapo hatutatafuta namna ya kupunguza gharama au kutoa nafuu katika kuunganisha umeme kwa watu," alisema.Hata hivyo, alisema mgawo wa umeme bado unaendelea nchini, ingawa kwa muda wa wiki moja sasa, kumekuwa na nafuu kidogo.
"Hii imetokana na maji kuongezeka katika mabwawa ya Kihansi na Kidatu kutokana na mvua zinazonyesha katika Milima ya Udzungwa. Kwa sababu hiyo, uzalishaji wa umeme katika mabwawa hayo umeongezeka kiasi na kuleta nafuu kidogo iliyopo sasa," alisema.
Lakini akatahadharisha kuwa ahueni hiyo si ya kutegemea sana, kwani hali katika Bwawa la Mtera bado siyo nzuri, hivyo siku yoyote mvua hizo zitakaposimama au kupungua katika Milima ya Udzungwa, mgawo utarudi kwa makali yake ya awali.
"Hadi leo nizungumzapo nanyi, kina cha maji katika Bwawa la Mtera kimefikia mita 690.88 ambacho bado ni chini sana. Maji yapo juu ya kina cha ukomo wa chini kwa sentimeta 88 tu, hivyo bado tuna safari ndefu mpaka kufikia kina cha juu cha mita 698," alisema.
Kuhusu mapato na matumizi ya Serikali, Rais alisema miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha (Julai – Desemba, 2010) makusanyo ya mapato ya Serikali yalikuwa chini ya lengo kwa asilimia nane.
Alisema hiyo imetokana na makusanyo katika Idara ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwa chini zaidi kwa kipindi hicho.Kuhusu nidhamu na matumizi ya fedha za Serikali Rais Kikwete ametaka wale wote wanaofanya vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali za umma na kukiuka sheria na kanuni za fedha na ununuzi wa umma, wachukuliwe hatua.
"Juhudi za kuongeza mapato ya Serikali zitakuwa na maana iwapo kutakuwa na matumizi mazuri ya fedha za Serikali," alisema na kuongeza:
"Jambo hili nimekuwa nalisisitiza mara kwa mara na nililirudia nilipozungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa."
Katika hatua nyingine, Rais alizungumzia maslahi ya watumishi wa umma akisema ni lazima wapate haki zao kwa wakati.Alisema watumishi kupandishwa cheo ni stahili yao na ni haki ya msingi. Hivyo, wakati wake unapofika na kama hakuna sababu za msingi lazima wapandishwe cheo.
Kuhusu Shirika la Reli Tanzania ((TRL) Rais Kikwete alihimiza uharakishaji wa mchakato wa kuachana na RITES na mchakato wa kuboresha reli ya Kati na TAZARA
No comments:
Post a Comment